Ninaamini kuwa umefika kwenye makala hii kwasababu tayari umesikia kuhusu jinsi juisi ya ukwaju inavyopunguza uzito haraka.
Watu wengi wanafahamu matumizi ya ukwaju katika kutengeneza vinywaji kama juisi ya ukwaju au katika kuongeza ladha kwenye chakula kama kutengeneza chachandu, sosi (sauce) au chutney nk.
Kwenye makala hii utaona faida nyingine nyingi za juisi ya ukwaju pia jinsi inavyosaidia kupunguza unene.
1. UKWAJU KAMA TIBA YA MATATIZO YA TUMBO.
Ukwaju unafahamika kuzuia vidonda vya tumbo vinavyosababishwa na dawa kama Ibuprofen.
Juisi ya ukwaju pia ina anti-oxidants ambazo husaidia kupunguza inflammation mwilini hivyo kulinda dhidi ya tatizo la inflammation linalotokea kwenye tumbo na utumbo.
INFLAMMATION NI NINI?
Inflammation ni tatizo linalotokea kwenye sehemu fulani ya mwili ambapo husababisha kutokea kwa ishara 5 kwenye sehemu iliyoathiriwa ambazo ni:
- Maumivu
- Kuongezeka joto
- Kubadilika kuwa na rangi nyekundu
- Kuvimba
- Kushindwa kusogeza mahala palipo husika mf inflammation kwenye goti husababisha ushindwe kusogeza mguu au kutembea vizuri.
Inflammation inaweza kusababishwa na vitu vilivyopo nje kama Kemikali.
Pia inaweza kusababishwa na infection pale vijidudu vinapoingia mwilini.
Chanzo kingine kikubwa cha inflammation ni mfumo wa kinga ya miili yetu.
Kwa kawaida mfumo wa kinga ya mwili hutengeneza sumu kwa ajili ya kuua vijidudu vinavyoingia mwilini ili kutulinda na magonjwa.
Sumu hii haitakiwi kutudhuru sisi bali wale wadudu wabaya.
Lakini kwa baadhi ya watu hutokea kuwa hiyo sumu inafanya kazi kwa wadudu huku pia ikiumiza sehemu za ndani ya mwili hivyo kusababisha inflammation.
Inflammation inaweza kutokea kwenye tumbo na utumbo kutokana na sababu mbalimbali kama vijidudu na pia kinga ya mwili.
Kwasababu ukwaju unafahamika kuwa na anti-oxidants ambazo husaidia kuzuia inflammation, huwa unatumika kuleta nafuu kwa watu wenye matatizo haya.
Matatizo ya inflammation ya tumbo na utumbo ni kama homa ya tumbo (Gastroenteritis), Crohn’s disease nk
2. UKWAJU KUTIBU CHOO NGUMU
Ukwaju una asidi inayoitwa Tartaric acid ambayo hufanya kazi sawa dawa zilizopo katika kundi la dawa aina ya Laxatives ambazo kazi zake kuu ni kutibu constipation.
Laxatives husaidia kuleta choo laini kwa kusababisha utumbo mpana unyonye maji kutoka mwilini na kulainisha choo wakati kikiwa kwenye utumbo mpana.
Pia Laxatives husaidia utumbo mpana kujikaza ili choo kipite kiurahisi.
3. JUICE YA UKWAJU NA KISUKARI
Inafahamika kwa watu wengi sana kwamba juisi ya ukwaju husaidia kucontrol sukari kwenye damu.
Hii ni kwasababu ukwaju una asidi inayoitwa Acetic acid ambayo huenda kujijumuisha kwenye mfumo wa asili wa mwili wa kucontrol sukari kwenye damu.
Watu wenye kisukari hupata unafuu kwa sababu ya hii tabia ya ukwaju kushusha sukari.
Lakini tahadhari inapaswa kuchukuliwa kwani sukari inaweza kushushwa sana hadi kuleta madhara pia.
4. JUISI YA UKWAJU KWA MAMA WAJAWAZITO
Kutokana na uchungu wake na tabia ya kuupa afya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, juisi ya ukwaju imekuwa ikitumika sehemu nyingi duniani kusaidia kupunguza tatizo la kichefuchefu na kutapika kwa wamama wajawazito.
5. JUISI YA UKWAJU NA KIFUA/MAFUA NA HOMA
Tafiti nyingi zimeonesha kuwa ukwaju una tabia sawa na dawa zinazoua vijidudu vinavyosababisha magonjwa mfano Bakteria na parasites wanaosababisha malaria. ( 1 , 2 3 )
Watu wengi hutumia juisi ya ukwaju mara tu mafua na kifua yanapotaka kuanza ili kuondoa kukereketa shingoni pia kuondoa homa.
6. JUISI YA UKWAJU KWA KINGA YA KISEYEYE
Kiseyeye ni ugonjwa unaoletwa na upungufu wa vitamin C mwilini.
Ukwaju una kiasi kikubwa wa vitamin C hivyo kukinga dhidi ya ugonjwa huu.
7. JUISI YA UKWAJU HUUA MINYOO YA TUMBONI
Watu wengi duniani wamekuwa wakiwapa watoto ukwaju ili kuua minyoo.
Tafiti za kisayansi zinakubaliana na hili na kuthibitisha kuwa kweli ukwaju hasa majani na gome la miti wake huua minyoo. ( 4 )
8. JUISI YA UKWAJU KAMA TIBA YA MATATIZO YA INI
Ukwaju una Vitamin A,B,C,E, K ambazo ni muhimu sana katika kuimarisha afya ya ini.
Una 12% ya vitamin B3 (Niacin) ambayo ni muhimu sana kwa ini.
Pia antioxidants zake kama Flavonoids, Vitamin C na Beta Carotene hufanya kazi pamoja kulinda ini.
9. JUISI YA UKWAJU NA AFYA YA MOYO NA MAUNGIO.
Antioxidants husaidia kuzuia inflammation kwenye moyo na mishipa mikuu inayopeleka damu kwenye moyo pamoja na maungio kama magoti nk
Pia ukwaju hupunguza kiasi cha mafuta na cholesterol kwenye damu pamoja na kushusha pressure ya damu hivyo kuzidi kuimarisha afya ya moyo. ( 5 )
10. JUISI YA UKWAJU NA MMENG’ENYO WA CHAKULA
Ukwaju unasaidia utengenezwaji wa nyongo mwilini ambayo ni muhimu sana katika kukamilisha mmeng’enyo wa chakula.
11. UKWAJU DHIDI YA KUKAUKA MACHO
Tatizo la kukauka macho huwapata watu wengi ambapo macho hushindwa kutengeneza machozi ya kutosha.
Kutokana na hili waathirika hujikuta wakipata maumivu sana wakifungua macho yao kana kwamba kuna mchanga ndani yake.
Mbegu ya ukwaju zina kemicali ambayo inafanana sana na ile inayotumika kutengeneza unyevu wenye kunata kwenye macho hivyo kusaidia kuondoa tatizo hili. ( 6 , 7 )
Zipo dawa nyingi za matone kwa ajili ya tatizo hili ambazo zimetengenezwa kwa mbegu za ukwaju. ( 8 )
12.UKWAJU NA VIDONDA VYA KUUNGUA
Kama tulivyoona mapema kwenye makala hii ukwaju unaweza kuua vijidudu kama bacteria na parasites.
Kwasababu vidonda vingi huweza kupata maambukizi ya vijidudu hivi kirahisi utumiaji wa ukwaju kwa kupaka eneo lililoungua mara baada ya tukio husaidia sana kuepusha maambukizi na kusababisha kupona haraka.
Pia ukwaju una kemikali zinazosaidia seli za mwili kuongezeka hivyo kupaka kwenye kidonda hufanya seli za ngozi kujitengeneza tena hivyo kuziba kidonda na ngozi kurudi katika hali ya zamani.
13. JUISI YA UKWAJU DHIDI YA CANCER
Kila wakati kwenye miili yetu kuna seli mpya zinazotengenezwa na kuna seli zilizozeeka zinazokufa ili kufanya mwili uwe na afya.
Cancer hutokea pale seli za mwili zinapozidi kuongezeka kasi isiyoya kawaida bila seli za zamani au zilizozeeka kufa.
Kwenye ukwaju kuna Polysaccharides ambazo huzuia cancer kwa kusababisha seli zilizozeeka zife ili seli mpya zifanye kazi kawaida.
14. JUISI YA UKWAJU INAVYOPUNGUZA UZITO
Ukwaju unasemekana kusaidia kupunguza uzito kwa njia kuu 2.
Kupunguza hamu ya kula:
Ukwaju una asidi inayojulikana kama Hydroxycitric acid (HCA).
Hii husaidia kupunguza uzito kwa kupunguza hamu ya kula hivyo kukuzuia kula kiasi kikubwa sana cha chakula kuliko mahitaji ya mwili wako.
Kupunguza mafuta mwilini:
HydroxyCitric acid pia hupunguza kasi ya uhifadhi wa mafuta mwilini kwa kuingilia kazi ya enzyme inayosababisha kubadilishwa kwa chakula kuwa mafuta mwilini (ATP Citrate lyase).
JINSI YA KUTENGENEZA JUISI YA UKWAJU
- Osha ukwaju kwa maji yanayotiririka kisha ondoa ganda la nje.
- Weka maji kiasi unachotaka kwenye sufuria kisha uchemshe ukwaju wako kwa dakika 10-15.
- Ipua kisha koroga ukwaju uwe kama uji uji.
- Chuja Juisi yako ya ukwaju na uweke sukari kidogo au asali.
- Hifadhi kwenye fridge tayari kwa kunywa.
JINSI YA KUNYWA JUISI YA UKWAJU KWA AJILI YA KUPUNGUZA UZITO
Watu wengi hudai kuona matokeo baada ya kunywa glasi moja kabla ya kila mlo.
Kuna watu ambao wapo sensitive sana kiasi cha kuwa hata nusu glasi inaweza kufanya waharishe sana.
Hakikisha unapata ushauri wa daktari wako kwanza pia sikiliza mwili wako, kama unaharisha sana basi punguza kiasi au ongeza maji kwenye juisi yako.
MAPUNGUFU YA VITHIBITISHO VYA JUU YA UKWAJU KUPUNGUZA UZITO
- HAKUNA TAFITI ZILIZOFANYWA KWA BINADAMU: Tafiti zote zilizofanywa juu ya jinsi juice ya ukwaju inavyopunguza unene zimefanywa aidha kwa PANYA au KUKU aina ya BROILER.
- JUISI YA UKWAJU HUSABABISHA KUHARISHA : Kwasababu ukwaju una tabia kama za dawa za laxative huwa unasababisha mtu apate choo laini sana mara nyingi kwa siku. Hii husababisha kutoka uchafu kwenye utumbo mpana hivyo kufanya mtu aonekane amepungua tumbo. Pia kuharisha husababisha kupunguza uzito wa maji mwilini. Hivyo inawezekana kunywa juice ya ukwaju kunasababisha kupungua haraka kwa sababu hii.
KWA KIFUPI:
Inawezekana ni kweli juice ya ukwaju husaidia kupunguza uzito hasa tumbo kutokana na upungufu wa uchafu kwenye utumbo mpana,upungufu wa maji pamoja na kupunguza kiasi cha chakula.
Lakini ni muhimu kukumbuka ukipunguza uzito haraka hasa kwa kuharisha una uwezekano wa zaidi ya 95% wa kurudisha uzito uliopoteza tena na nyongeza ndani ya muda mfupi pia.
Kazi ya ukwaju katika kupunguza utengenezwaji mafuta yanayokaa chini ya ngozi umeonekana kuwa ni ya muda mfupi tu na kiasi kinachozuiwa ni kidogo.
Itabidi tafiti mpya zifanywe kwa binadamu ili kuhakikisha kama kweli diet ya juice ya ukwaju husababisha kupunguza uzito kwa binadamu.
TAHADHARI: MADHARA YA JUISI YA UKWAJU
1.Watu wenye kisukari, wamama wajawazito, wamama wanaonyonyesha na watu wanaokaribia kufanyiwa operation wapate ushauri wa daktari kabla ya kunywa juisi ya ukwaju.
2.Usitumie juisi ya ukwaju ukiwa katika dozi ya ASPIRIN au IBUPROFEN kwasababu ukwaju hufanya kiasi kikubwa kuliko kawaida cha hii dawa kuingia kwenye damu hivyo kufanya usikie zaidi yale madhara ya hizo dawa.
Mwisho kabisa faida za kunywa juice ya ukwaju ni nyingi sana kwa hiyo hata kama ni kweli inasaidia kupunguza uzito au la ni kinywaji kizuri kwa afya.
Cha muhimu ni kukumbuka kutotegemea mbinu fupi za haraka za kupunguza uzito.
Badala yake ni muhimu kufata njia na misingi sahihi ya kupunguza unene ambayo ni lishe sahihi na mazoezi ya viungo.
Je umewahi kutumia juice ya ukwaju kwa ajili ya kupunguza uzito? Matokeo yako yalikuwaje?
0 Comments